Mashabiki na wanachama wa Young Africans wameombwa kusahau yaliyopita na kuelekeza mawazo yao katika mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Wolaita Dicha kutoka Ethiopia, utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.
Wito huo kwa wanachama na mashabiki wa Young Africans umetolewa na mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Young Africans Dismas Ten, baada ya kuchafuka kwa hali ya hewa klabuni hapo, kufuatia kikosi chao kuondolewa kwenye michuano ya kombe la shirikisho (ASFC), dhidi ya Singida Utd.
Young Africans ilitupwa nje ya michuano ya FA na Singida United kwa mikwaju ya penati 4-2 Aprili mosi baada ya kutoka sare ya bao moja katika muda wa kawaida.
Dismas Ten amesema kila mwanachama na shabiki wa klabu hiyo hana budi kuungana na kikosi katika kipindi hiki cha maandalizi ya kuelekea mchezo wao wa jumamosi, ili kufikia lengo la kupata ushindi nyumbani, kabla ya kuelekea nchini Ethiopia kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili.
“Kikubwa ninawaomba mashabiki wa Young Africans kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi kuipa sapoti timu wakiwa na jezi zao za kijani ili kuhakikisha tunashinda hapa nyumbani,” alisema Ten.
Wakati huo huo Young Africans imetangaza viingilio vya mchezo wao dhidi ya Wolaita Dicha ya Ethiopia, huku kiingilio cha chini kikiwa shilingi elfu tatu (3000).
Viingilio vingine kwa upande wa VIP A ni sh 15,000, VIP B na C sh 10,000. Young Africans imeweka viingilio hivyo rafiki ili kuwafanya mashabiki wengi kujitokeza kuwapa sapoti wachezaji uwanjani.
Katika mchezo huo Young Africans itawakosa huduma za wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi, Obrey Chirwa na Said Makapu ambao wana kadi mbili za njano kila mmoja.