Mashambulizi yaliyofanywa hivi karibuni na vikosi vya jeshi la Marekani vinavyosaidia harakati za jeshi linalopambana na Serikali ya Syria, yamewaua wanajeshi kadhaa wa Urusi nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na CNN, vikosi vya Marekani vilianzisha mashambulizi yaliyotumia ndege maalum katika eneo ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na ISIS kabla ya kunyang’anywa. Eneo hilo linalojulikana kama Coneco lina mafuta na gesi pamoja na kiwanda cha nishati hizo.
Katika mapambano hayo ambayo yalidumu kwa saa tatu mfululizo, imeelezwa kuwa wanajeshi kadhaa wa Urusi waliokuwa wanafanya kazi na shirika la Wagner waliuawa.
Mwanaharakati, Ruslan Leviev anayefanya kazi jijini Moscow nchini Urusi alisema kuwa namba ya raia wa Urusi waliokufa kwenye tukio hilo ni kati ya 20-30.
Alisema kuwa inaonekana watu hao walitumwa katika eneo hilo bila kupewa ulinzi wa ndege za kivita.
Hata hivyo, Msemaji wa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Maria Zakharova alisema kuwa idadi ya raia wa Urusi waliouawa nchini Syria ni watano pekee.
Marekani na Urusi wamekuwa na mgongano katika mgogoro wa Syria, Marekani ikiwaunga mkono wanajeshi wanaopambana dhidi ya Serikali ya Rais Bashar Al Asaad ambaye anaungwa mkono na Urusi.