Ariana Grande amewapa mtihani mgumu waandishi wa habari nchini Marekani, wanaotaka kuchukua matukio ya ziara yake mpya ya ‘Sweetener World Tour’, hali iliyosababisha vyombo vingi vya habari kutishia kususia kuandika habari zake.
Mwimbaji huyo amesema kuwa kwa waandishi wa habari wanaotaka kuchukua matukio ya ziara hiyo wanapaswa kusaini mkataba maalum ambao utaweka masharti ya namna picha zake zitakavyopigwa na hata kutumika.
Kwa mujibu wa TMZ, ameeleza kuwa waandishi watakaosaini mkataba huo watatakiwa kupiga picha za mnato tu lakini pia wataruhusiwa kupiga picha hizo kwenye nyimbo tatu tu za mwanzo katika kila tamasha.
Aidha, wapiga picha wote wanapaswa kukubaliana na sharti la ‘work-made-hire’, ambapo lina maanisha kuwa picha zote zinazopigwa ni lazima mpiga picha ahamishe haki miliki kwenda kwa kampuni ya Ariana Grande.
Masharti hayo yamepingwa vikali na vyombo vya habari kama vile New York Times, La Times na Shirika la Habari la AP, wakieleza kuwa ni hatua ya kuidhalilisha taaluma ya habari.
“Masharti aliyotoa Ariana ni kuidhalilisha taaluma na hayakubaliki. Tunamtaka ayaondoe mashariti hayo na sisi tutafuata miiko ya uandishi wa habari katika kufanya kazi ya kuripoti ziara hiyo,” linaeleza tamko la Chama cha Wapiga Picha wa Marekani kiitwacho ‘National Press Photographers Association’ (NPPA).
Vyanzo vyenye uhusiano wa karibu na mwimbaji huyo vimeeleza kuwa uamuzi wake umetokana na jinsi ambavyo wapiga picha wengi walivyotumia picha za matamasha yake ya awali kufanyia biashara, tofauti na makubaliano ya kuzitumia kwa ajili ya habari tu.
Imeelezwa kuwa wapiga picha wa matamasha yake walikuwa wakizitumia kuandaa kalenda, vitabu na machapisho mbalimbali na kuyauza.