Mashindano ya vikundi vya kufanya mazoezi yanatarajiwa kuanza hivi karibuni jijini Dar es salaam na mikoa mingine ili kutekeleza kauli na agizo la Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati anazindua kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi Desemba 17 2016.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, wakati wa ufunguzi wa mazoezi ya hiari Mkoa wa Dar es salaam yaliyofanyika katika wilaya ya Temeke.
“Hata kama zawadi ikiwa ng’ombe lazima kipatikane kikundi kimoja cha mazoezi ambacho ni bora kuliko vikundi vingine mkoa mpaka kitaifa ili kuwafanya watanzania waepuke magonjwa yasioambukiza kwa kupenda mazoezi.
Ummy amesema kuwa kampeni hiyo ya kufanya mazoezi inalenga zaidi kupunguza gharama za kutibu ugonjwa huo na badala yake kuwataka watazania kufanya mazoezi siku tatu katika wiki angalau kwa dakika 30 il kujikinga na magonjwa yasiomabukiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amesema kuwa mazoezi hayo yamewahamasisha na wamepanga kila ijumaa wafanyakazi wote wa umma wanatakiwa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.