Kampuni 28 za Serikali likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania – TPDC na Shirika la Madini la Taifa – STAMICO zinatarajia kuwekwa huru na kuachana na utegemezi wa Serikali.
Hayo yamebainishwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu wakati akiongea kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Mwenyekiti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma katika ukumbi wa Mikutano wa AICC jijini Arusha.
Amesema, Taasisi hizo ambazo majina yake yote hayajawekwa hadharani ni pamoja na Vyuo 13 vya Elimu ya Juu vya Umma ikiwa ni matokeo ya mabadiliko yanayoendelea katika taasisi za umma nchini.
“Tumefikia muafaka na Wenyeviti na Wakurugenzi wa taasisi hizi. Tunataka kuona makampuni mengi yanafanya kazi kwa uhuru, baadhi ya taasisi hata hivyo zimeomba kuongezewa muda wa hadi miaka miwili ili kuwa huru kikamilifu,” alisema Mchechu.