Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema azma ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya kuanzisha Mashirika ya umma ni kutaka yamilikiwe na Wananchi kupitia hisa.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Agosti 19, 2023 mara baada ya kufungua Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi hizo, kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha.
Amesema, “Nataka niseme kidogo kuhusu azma ya kuanzisha mashirika haya ya umma. Wakati wa Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Mashirika haya ya umma, alitaka yamilikiwe na wananchi wenyewe kupitia hisa kama Public Enterprises na sio government enterprises.”
“Tunajiita Mashirika ya Umma lakini dhana ya Mashirika ya Umma, ni mashirika ambayo umma Watanzania wana hisa katika mashirika yale,” amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.