Serikali imeyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kuzingatia maadili ya nchi wakati wa utekelezaji wa afua mbalimbali. na kutokubali kutumika kuwa chombo cha kuhamasisha mmomonyoko wa maadili ya Taifa na kwamba watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia mkataba uliopo na utaratibu wa nchi.
Raia hiyo, imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua mpango huo jijini Dar es Salaam wa kuanzia mwaka 2023 hadi 2030, ili kuelekea katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia 2030, unaotarajia kugharimu dola la kimarekani milioni 458 kwa miaka nane.
Amesema, anazitaka Mamlaka zote za Serikali zinazohusika na usajili wa mashirika yasiyo ya Kiserikali kufuatilia kwa karibu utendaji wa mashirika hayo ili kuzuia mianya ya kuhamasisha vitendo vya mmonyoko wa maadili na kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta Afya.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ambaye alimuwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali inatambua mchango wa asasi zisizo za Kiserikali kusaidia kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi na itaendelea kuweka sera na mipango madhubuti, ili kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi la Shirika la AMREF Tanzania Anthony Chamangwana amesema kuwa Amref itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuwafikia wananchi kwa idadi kubwa zaidi na wanufaike na huduma bora za afya kuanzia ngazi ya jamii hadi ngazi ya Taifa.