Baada ya wiki kadhaa, hatimaye Baraza la Wawakilishi linataraji kupiga kura leo Jumatano kupeleka mashtaka dhidi ya Donald Trump mbele ya Bunge la Seneti.
Hii ni hatua ya mwisho kabla ya kuanza kwa kesi ya ung’atuzi dhidi ya rais huyo kutoka chama cha Republican.
Spika wa Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Democratic na mpinzani mkuu wa Donald Trump katika baraza hilo, Nancy Pelosi, alitangaza Jumanne wiki hii baada ya mkutano faragha na wabunge kwamba mashtaka yanayomkabili Donald Trump yatapelekwa mbele ya Bunge la Seneti leo Jumatano Januari 15.
Bunge la seneti linadhibitiwa na chama cha Republican cha Donald Trump.
Wadadisi wanasema ni vigumu bunge hilo lipitishe mashitaka hayo ya rais kutoka chama kinachodhibiti taasisi hiyo kubwa nchini Marekani.
Donald Trump anakabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuzuia Bunge kufanya shughuli zake.
Upinzani unaamini kwamba Rais Donald Trump alitumia rasilimali za serikali kushinikiza Ukraine kuchunguza mgombea urais kutoka chama cha Democratic Joe Biden, mpinzani wake katika uchaguzi wa urais wa Novemba.
Upinzani unamshtumu haswa kwamba alizuia msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo iliyo katika mgogoro wa kijeshi na jirani yake Urusi, ili kufanikisha malengo yake.