Klabu ya Mashujaa FC imetangaza rasmi kuwa itapiga kambi yake mjini Zanzibar kujiandaa na msimu mpya wa mshindano, huku ikiendelea kufanya usajili wa kukiimarisha kikosi chake.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo itakayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu ujao, imeeleza kuwa kambi hiyo inatarajiwa kuanza Jumatano juma hili.
“Tunapenda kuwataarifu kwamba, maandalizi ya msimu ujao kwa klabu yetu yatafanyikia visiwani Zanzibar kuanzia Julai 19,” imeeleza taarifa hiyo.
Mashujaa yenye maskani yake Kigoma, ní moja kati ya timu tatu mpya ambazo msimu huu zitacheza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Zingine ni JKT Tanzania ambayo ilikuwapo misimu kadhaa iliyopita kabla ya kushuka daraja na sasa imerejea pamoja na Tabora United ambayo ilipanda kwa jina la Kitayosce kabla ya kuamua kubadilisha jina hilo.
Wakati hayo yakiendelea Mashujaa imeendelea kujiimarisha kwa kufanya usajili, ambapo imemsajili kipa aliyewasumbua mno kwenye mechi ya ‘play off’, Lameck Kanyonga wa Mbeya City, pamoja na kipa mwingine Lukumbiza Pascal kutoka Pamba FC.
Wengine ni Mshambuliaji Kelvin George kutoka Bumamuru FC ya Burundi, Omari Kindamba, Nassor Kiziwa kutoka Mtibwa Sugar, Abdul-nasir Asaa Mohamed ‘Gamal’ kutoka Mlandege na Adam Adam kutoka Ihefu FC.