Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ ameeleza kuwa timu hiyo inahitaji wachezaji bora zaidi kwa ajili ya kupata ushindi, hivyo anatarajia kulitumia dirisha dogo kusajili wachezaji bora zaidi kuimarisha kikosi chao.
Hayo yameelezwa na kocha huyo baada ya timu yake kupoteza mchezo wa pili mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wake wa nyumbani baada ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Singida Big Stars.
“Mashujaa bado inahitaji kuunda timu bora na wachezaji bora, lazima tutembee sehemu mbalimbali huko nje na ndani ya nchi kuona mchezaji gani atatufaa.
“Maana ukiangalia mbinu kila siku zinaenda vizuri, kwa sababu ukifundisha timu na kufika sehemu ya mwisho ya umaliziaji maana yake timu inakuwa tayari imekamilika, lakini tatizo linakuwa ni kwa mtu mmoja mmoja kuamua,” amesema Baresi.
Kwa matokeo hayo, kocha msaidizi wa Singida, Thabo Senong amesema: “Kila timu, kila mechi ni ngumu lakini kwenye mechi iliyopita tuliangalia zaidi utendaji wa kazi uwanjani.”
Mashujaa sasa inashika nafasi ya 10 ikiwa na alama nane baada mechi ya nane wakati Singida ipo nafasi ya saba kwa alama 12 baada ya kushuka dimbani mara tisa.