Wageni wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mashujaa FC ya mkoani Kigoma, imemaliza maandalizi ya msimu mpya na imesema kwa sasa ipo tayari kwa vita ya ligi hiyo itakayoicheza kwa mara ya kwanza.
Mashujaa imepanda daraja kutoka Ligi ya Championiship ikipitia kwenye mechi za Play-Off dhidi ya Mbeya City na ilianza maandalizi ya msimu mpya kwa kuboresha benchi la ufundi ikimtambulisha Abdallah Bares na kusajili wachezaji wengine wapya.
Akizungumzia maandalizi ya msimu mpya, Kocha Bares amethibitisha kuwa tayari na sasa wanasubiri kipyenga kipulizwe, kazi ianze.
“Kwa kiasi Kikubwa tumejenga timu kwa namna kwani tunataka kucheza soka la ushindani, tuna mchanganyiko wa wachezaji wageni kwenye Ligi Kuu na wazoefu. Hilo litatusaidia,” alisema Bares aliyetua kikosini hapo akitokea Tanzania Prisons na kuongeza;
“Tupo tayari kwa mapambano, kwa muda mrefu Kigoma haikuwa na timu ya Ligi Kuu lakini sasa imepatikana hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yao, na sisi tupo tayari kuwafurahisha.”
Mashujaa mechi zake tatu za mwanzo zote itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa LakeTanganyika ikianza Agosti l6 dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 21 dhidi ya Geita kisha Septemba l6 itakapovaana na lhefu.