Kikosi cha Mashujaa FC cha mkoani Kigoma kimesema kimejipanga vyema kwa ajili ya kusaka matokeo chanya katika kila mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara watakayocheza msimu huu 2023/24.
Mashujaa FC walianza vizuri msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/2024 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na kutoka suluhu iliyokutana na Geita Gold FC.
Akizungumza mjini Kigoma, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohammed ‘Bares’ amesema anahitaji kuvuna pointi ama katika mechi ya nyumbani au ugenini kwa sababu anahitaji kumaliza katika nafasi za juu.
Bares amesema anatambua ligi ya msimu huu inaushindani lakini mipango waliojiweka ni kushinda kila mechi watakayocheza na hatimaye kufikia malengo.
Amesema wamekuja katika Ligi Kuu Bara kuonyesha Ushindani na matarajio yake makubwa ni kuendelea kasi waliyoanza nayo bila kuwadharau wapinzani wao.
“Tumeanza msimu vizuri, matarajio yangu ni kuona kasi tuliyoanzanayo iwe zaidi katika mechi zijazo, tunapoelekea ligi inazidi kuwa ngumu. Mipango yetu ni kufanya vizuri na kuleta ushindani katika ligi hii ili kufikia malengo, mipango hii ni lazima kushinda mechi za nyumbani na ugenini,” amesema Bares.
Ameongeza siku 20 ambazo hawatacheza mechi, wachezaji amewapa mapumziko ya siku nne na siku zilizosalia wataendelea kubakia Kigoma kuendelea na mazoezi.
“Tutakuwa na mapumziko ya siku chache, kwa msingi huo wachezaji watabaki kambini (Kigoma), kwa sababu hatukuwa na muda wa kufanya maandalizi tofauti, tutatumia muda huu kuyafanyia kazi mapungufu ya kikosi changu nililyoyaona katika mechi mbili tulizocheza,” amesema Bares.
Hata hivyo ameongeza wanaweza kwenda Burundi au kualika timu kutoka taifa hilo kwa ajili ya kupata mechi za kirafiki za kujipima kabla ya kuwakabili Ihefu ya Mbeya.
Mashujaa FC watakuwa wenyeji dhidi ya Ihefu FC katika mechi ya raundi ya tatUu ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Septemba 16 mwaka huu kwenye dimba la Lake Tanganyika, Kigoma.