Katika hali inayoonyesha Mashujaa FC iliyopanda daraja msimu huu imejipanga vyema, imefanikiwa kumsajili Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Nassor Kiziwa, kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hiyo ni siku moja baada ya kumtambulisha mchezaji mwingine, Michael Masinda, kutoka Prisons pamoja na Kocha Mkuu, Mohamed Abdallah ‘Bares.’
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesema wanaamini usajili wa Kisiwa utakisaidia kikosi chao kufanya vizuri katika msimu ujao utakaoanza Agosti 15, mwaka huu.
Usajili huo ni moja kati ya maagizo ya Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, aliyewataka wabunge, wafanyabiashara na wasanii kutoka Kigoma kuichangia klabu hiyo kwa hali na mali ili kusajili wachezaji wazuri.
“Tuitie moyo timu yetu ili ikashindane, siyo kila siku kuziangalia Simba na Young Africans kwenye TV, tunataka waje hapa, waje Lake Tanganyika…lakini kukarabati uwanja wetu ufanane na Kigoma tunayotaka kuijenga.”