Kikosi cha Mashujaa FC kimerejea mazoezini na moja kwa moja kimepelekwa kwenye fukwe za ziwa Tanganyika, Kigoma kwa ajili ya mazoezi ya kurudisha utimamu wa mwili na pumzi kabla ya kuanza raundi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mohamned Abdallah ‘Bares’, amesema baada ya mapumziko ni lazima awarejeshee nguvu na pumzi wachezaji wake, hivyo ameanza kwenye fukwe za ziwa hilo hadi pale atakapoona wameiva na baada ya hapo atawa- hamishia uwanjani.
“Tuliwapa mapumziko wachezaji wetu, lakini kwa sasa wamerejea na tumeanza kujifua kwenye fukwe za ziwa Tanganyika hapa Kigoma, nadhani tuna majuma matatu za mapumziko ya Kalenda ya FIFA, kwa hiyo zinatosha sana kuwafanyisha mazoezi hapa ya utimamu wa mwili, baadaye turudi uwanjani,” amesema.
Hata hivyo, Bares amesisitiza kuwa anahitaji mechi angalau tatu za kirafi ki na hasa akizilenga timu za nchini Burundi kwa ajili ya kuipa timu yake ushindani.
“Kwangu mimi nahitaji mechi tatu, zinatosha sana, ila nataka zile zenye ushindani na tumeona ndugu zetu wa Burundi timu zao nazo zinajiandaa kwa ajili ya ligi wanaitikia wito wa kutaka kucheza na sisi mechi za kirafiki, kwa hiyo ningependa kucheza na timu za huko, kama itapatikana nafasi ya wao kuja sawa, lakini sisi wenyewe tunaweza kwenda huko kucheza,” amesema.
Mpaka sasa Mashujaa iliyopanda daraja na kuanza kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, haijapoteza mechi yoyote, ikishinda mchezo wa kwanza mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na suluhu dhidi ya Geita Gold FC.
Mashujaa inatarajiwa kucheza dhidi ya Ihefu, Septemba 16, mwaka huu na bado itaendelea kuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, Lake Tanganyika, Kigoma, kwa mechi ya tatu mfululizo.