Baada ya Pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/23 kufungwa rasmi jana Ijumaa (Juni 09) kwa Young Africans kukabidhiwa taji la ubingwa na sasa Mashujaa inapiga hesabu za kucheza ligi hiyo kupitia mtoano (play-off), ikisema ipo tayari kukutana na timu yoyote kwenye hatua hiyo.
Mashujaa kutoka Ligi ya Championship ndio itakayopambana na timu moja kutoka Ligi Kuu ili kuwania kupanda daraja msimu ujao kuungana na JKT Tanzania na Kitayosce na kocha wa timu hiyo kutoka Kigoma, Rashid Idd ‘Chama’ amesema wapo tayari.
Chama amesema wanaendelea kujinoa kwa ajili ya michezo miwili ya mtoano wakijua kutakuwa na ushindani mkubwa. “Tumeendelea na mazoezi tangu tulipomaliza michezo yetu ya hatua ya mtoano dhidi ya Pamba na kikosi kipo vyema kwa ajili ya kupambania nafasi ya kwenda Ligi Kuu.
“Tunajua utakuwa ushindani mkubwa kutokana na wapinzani wetu ndio kwanza wanatoka kumaliza ligi ya kuendelea yao, hivyo hakutakuwa na maandalizi zaidi pale walipoishia,” amesema Chama
Amesema mojawapo wa malengo yao msimu ujao ni kuhakikisha wanapanda Ligi Kuu.
Mashujaa FC itacheza na mshindi wa jumla wa mchezo wa Paly Off wa Ligi Kuu kati ya KMC FC iliyomaliza nafasi ya 13 dhidi ya Mbeya City iliyomaliza nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi hiyo.