Imefahamika kuwa madai ya Maslahi Makubwa yaliyowasilishwa na Kocha Denis Kitambi ndio sababu kuu iliyopelekea kuachana na klabu Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Juzi Jumanne (Desemba 12) Uongozi wa Namungo FC kupitia vynazo vya habari vya klabu hiyo ulithibitisha kuachana na Kocha huyo mzawa ambaye alikabidhiwa timu, baada ya kuondoka kwa Cedric Kaze, aliyetangaza kujiuzulu mwezi Oktoba.
Katibu Mkuu wa Namungo FC, Ally Seleman amesema wameamua kuachana na Kitambi kutokana na kushindwa kuafikiana katika maslahi ya mkataba mpya.
“Ni kweli tumeachana na Kitambi, aliomba kuboreshewa maslahi yake katika mkataba mpya lakini kiasi alichohitaji hatukuwa na uwezo nacho hivyo ameamua kuondoka na sisi tumemruhusu na kumtakia mafanikio huko anakoelekea,” amesema Seleman
Amesema kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Shedrack Nsajigwa huku wakiendelea na mchakato wa kumsaka kocha mpya.
Seleman amesema amepanga kuharakisha mchakato huo ili kuifanya timu iendelee kupata matokeo mazuri katika mechi zinazowakabili za Ligi Kuu na mashindano ya Kombe la FA.
Kitambi anakuwa kocha wa pili kuondoka Namungo msimu huu baada ya Cedric Kaze ambaye alijiondoa mwenyewe kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya aliyokuwa akiyapata.