Aliyekuwa Kocha wa Simba SC na Dodoma Jiji FC, Masoud Djuma, amemwaga sifa za kutosha kwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Andre Essomba Willy Onana akisema ni mtu hatari uwanjani.
Onana amesajiliwa Simba SC akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambapo alikuwa na mafanikio makubwa baada ya kumaliza ligi akiwa kinara kwa kutupia mabao 16.
Akizungumza kutoka kwao Burundi Masoud Djuma amesema kuwa Onana ni mchezaji hatari sana na anastaili nyingi za uchezaji bora zaidi ya Saido Ntibazonkiza na Pape Sakho.
“Onana ni msikivu sana ila pia ni hatari sana uwanjani hasa kwa kufunga, ila pia ni msikivu sana linapokuja suala la maelekezo kwa kocha hivyo ninaimani atafanya vizuri sana kwa Simba SC.” amesema Masoud.
Wakati huo huo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema wanaamini kuwa wamefanya usajili wa mchezaji mkubwa na mzuri ambaye anaweza kucheza nafasi nyingi bila kusahau kutupia mabao na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.
“Onana ni moja kati ya usajili mzuri na usajili mkubwa kufanywa na timu zote za Tanzania kwa msimu huu, mchezaji akiwa anatoka katika nchi ya mpira kama Cameroon basi ni wazi kuwa ni bonge la mchezaji.
“Baada ya Simba SC kumpata mchezaji huyo natamani hata ligi ianze leo kutokana na kuwa na shauku ya kumuona fundi huyu ambaye naamini atakuja kuipa Simba nguvu na kufanya vyema katika kila michuano ambayo tutashiriki,” amesema kiongozi huyo.