Kikosi cha Simba kilichokuwa nchini Djibout kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kimewasili usiku wa kuamkia leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari uwanjani hapo, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma amesema kila kitu kilikwenda vizuri nchini Djibout, huku akiweka wazi kuwa hawakutaka kuweka nguvu nyingi kwenye mchezo huo kutokana na ushindi mkubwa wa mabao 4-0 walioupata kwenye mchezo wa kwanza, hivyo walikuwa wakihifadhi nguvu kwa ajili ya michezo iliyo mbele yao.
Katika mchezo huo wa marudiano, Simba imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gendramerie, bao likifungwa na Emmanuel Okwi, na hivyo kufuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 5-0, na itakutana na Al Masry ya Misri.
Alipoulizwa kuhusu jinsi walivyojiandaa kuwakabili Al Masry, Masoud amegoma kuwazungumzia wapinzani wao hao wa michuano hiyo ya Afrika, akidai kuwa muda wa kuwazungumzia bado haujafika, lakini akasisitiza hakuna wanachoogopa.
Masoud amesema wanachoangalia kwa sasa ni mchezo ulio mbele yao ambao dhidi ya Mbao Fc utakaopigwa Jumatatu Februari 26 mwaka huu katika dimba la Taifa Dar es Salaam.
“Kwa sasa hatuangalii Misri, ligi ni muhimu zaidi kuliko Misri, kwanza tunajiandaa na Mbao. Hatuna chaguo jingine la kufanya, lazima tuifunge Mbao maana tumebakiwa na nafasi moja tu hiyo ya ligi,” amesema Maoud.
Kuhusu hali ya John Bocco ambaye ni majeruh, Masoud amesema mchezaji huyo ambaye ndiye nahodha wa Simba, anaendelea vizuri na kuna matumaini makubwa ya kucheza katika mchezo dhidi ya Mbao FC.