Vita ya kurithi kiti cha Arsene Wenger huko kaskazini mwa jijini London imeendelea kupamba moto, baada ya babu huyo kutoa mkono wa kwaheri kwa mashabiki wa klabu hiyo jana jioni.
Wenger ataondoka Emirates Stadium mwishoni mwa msimu huu, baada ya kuitumikia klabu ya Arsenal kwa kipindi cha miaka 22, na kuwa meneja aliedumu kwa muda mrefu na klabu moja katika ligi kuu ya England.
Hadi hii leo majina ya Massimiliano Allegri (meneja wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus) na Luis Enrique aliekua meneja wa FC Barcelona yamekuwa yakipewa nafasi kubwa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha babu huyo kutoka nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports, wawili hao wanaonekana kuchuana katika vita hiyo, na tayari wameanza kujadiliwa katika vikao vya ndani vya uongozi wa klabu ya Arsenal.
Allegri, amesaliwa na mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Juventus, na tayari msimu huu ameiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa nne wa ligi ya Italia.
Endapo Arsenal watafanya maamuzi ya kumpa ajira Allegri, watalazimika kuvunja mkataba wake huko mjini Turin, na itawagharimu kiasi kikubwa cha pesa.
Kwa upande wa Enrique ambaye tayari ameshapumzika kwa msimu mmoja baada ya kuondoka Camp Nou mwishoni mwa msimu uliopita, yupo tayari kurejea katika shughuli za ukufunzi na amedhamiria kubadili mazingira ya utendaji kazi.
Enrique hatoigharimu chochote Arsenal endapo atatua Emirates kuchukua nafasi ya Arsene Wenger, kutokana na kuwa huru katika kipindi hiki.
Wengine wanaotajwa katika mbio za kuwania kiti cha Arsene Wenger ni Carlo Ancelotti, Zeljko Buvac (msaidizi wa Klopp) pamoja na Mikel Arteta ambaye kwa sasa ni msaidizi wa Pep Guardiola.