Christome Simon (47), mkazi wa Mtaa wa Kambi tano kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro anayedaiwa kupotea tangu Novemba, 2022 na mabaki ya mwili wake kukutwa msitu wa Mgulu wa Ndege uliopo katika mtaa huo ameacha maswali mengi kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Joachim Simon amesema ndugu yake alipotea kwa mazingira ya kutatanisha na mara ya mwisho alionekana katika mtaa huo akiwa amevaa begi baada ya hapo hakupatikana licha ya kupiga simu yake na kumtafuta maeneo mbalimbali na bado hawajui nini kilimsibu.
Akisimulia tukio hilo, Joachim amesema Juni 21, 2023 alipata taarifa kua kuna mabaki ya mtu msituni ndipo alipokwenda na kufanya uchunguzi akabaini kuwa ni ndugu yake kupitia simu yake, nguo na viatu alivyokua amevaa na hivyo kupata simanzi na kujiuliza maswali mengi.
Anasema, “nilipokua shambani akaja kijana mmoja, akasema wakati anafukuza nyani Mbwa wakawa wanabweka, alipoenda akakuta mabaki ya mtu, nikaondoka nilipofika nikagundua ni kweli ndugu yangu kupitia simu yake licha na kua inakutu, nguo na viatu vyake.”
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa Lukobe, Eliamin Kimaro amesema kwa kushirikiana na Polisi walifika na kuchukua mabaki hayo kukabidhi kwa ndugu husika huku jamii ya eneo hilo ikiendelea kutafakari juu ya tukio hilo la kushangaza ambalo limeacha maswali yasiyo na majibu.