Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya kwenda kwa Shirika la Msaada la Marekani (USAID) imepiga marufuku kutoa matangazo yanayohusu masuala ya uzazi wa mpango katika vyombo vya habari yanayorushwa kwenye runinga na redio mbalimbali nchini mpaka itakapotangazwa tena.
USAID ndiyo Shirika linalofadhili mradi wa Tulonge Afya unaotoa matangazo hayo ya kuhamasisha uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari.
Barua hiyo imeeleza kuwa serikali inatambua mchango na juhudi za shirika hilo katika kuboresha uzazi wa mpango hivyo wizara inakusudia kufanya marejeo ya maudhui yote ya matangazo kwenye runinga na redio kwa ajili ya uzazi wa mpango.
“Hivyo unaombwa kusimamisha mara moja kutangaza na kuchapisha maudhui yeyote yale ya uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari mpaka itakavyoamuliwa vinginevyo,”inaeleza taarifa hiyo.
Wizara imefikia uamuzi huo kufuatia hotuba ya Rais John Pombe Magufuli iliyofanyika Septemba 9, mjini Meatu Mkoani Simiyu, aliposema Watanzania waendelee kuzaa, lakini wachape kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wanaowazaa na kudai kuwa watu wanaopanga idadi ya watoto ni wavivu wa kufanya kazi.