Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, kupitia elimu ya Polisi jamii iliyotolewa Kata ya Mzeze Wilaya ya Kipolisi Manyovu, limewahamasisha Wananchi kuwafichua Matapeli wanaojihusisha na ramli chonganishi, kufuatia uwepo wa Waganga wa jadi maarufu kama lambalamba mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi wa Polisi – ACP, Filemon Makungu amesema Waganga hao wamekuwa wakiwadanganya wananchi kwamba wanauwezo wa kuwafichua watu wanaojihusisha na imani za kishirikina au wachawi, kitendo ambacho ni uongo na kinachozua taharuki kwa jamii.
Amesema, ramli chonganishi ni chanzo cha migogoro na uhalifu ndani ya jamii ikiwepo mauaji, ukatili wa kijinsia, familia kusambaratika na chuki na kwamba vitendo hivyo vinatakiwa kukemewa na kuondolewa ndani ya jamii kwa ushirikiano baina Jeshi la Polisi na jamii.
Aidha, ACP Makungu ameihamasisha jamii kutowapokea na kuwahifadhi wahamiaji wanaoingia na kuishi nchini kinyume na sheria, huku Wananchi wa Kata hiyo wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwaripoti waganga matapeli ikiwemo waganga matapeli, ili wachukuliwe hatua za kisheria.