Kocha Mkuu wa Mbeya City FC Mathias Lule amesema kufanya vibaya kwa kikosi chake katika siku za karibuni kunatokana na wachazaji wa klabu hiyo kujisahau.
Mbeya City FC imeshindwa kufurukuta katika michezo sita iliyopita, kabla ya kuangukia pua jana Jumamosi (April 02), kwa kufungwa 1-0 na Geita Gold katika Uwanja wake wa nyumbani Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Kocha Lule raia wa Uganda amesema, asilimia kubwa ya wachezaji wa Tanzania wanapopata matokeo mazuri mfululizo huwa wanajisahau, na kuona wameshamaliza kila kitu, jambo ambalo limeisibu timu yake katika kipindi hiki.
“Tatizo la wachezaji wengi wa vilabu vya Tanzania pale wanapopata ushindi mfululizo basi huwa wanasahau kuendelea kupambana ili wapate ushindi zaidi na zaidi” amesema Kocha Lule
Kabla ya kupoteza mchezo wa jana Jumamosi (April 02) dhidi ya Geita Gold, Mbeya City FC ilipoteza dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wake wa nyumbani kwa kufungwa 1-0.
Kwa matokeo hayo Mbeya City FC ambayo ilikua na mwanzo mzuri msimu huu, inaendelea kuwa katika nafasi ya 05 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 25, zilizopatikana kwenye michezo 19 waliocheza hadi sasa.