Matokeo ya kidato cha nne yametoa picha ya kipekee mwaka huu baada ya Mtanzania mwenye asili ya China, Congcong kushika nafasi ya pili kitaifa huku akifanya vizuri zaidi kwenye somo la Kiswahili.
Congcong ambaye Mtanzania mwenye asili ya Kichina, alizaliwa nchini lakini wazazi wake ni raia wa China, amesoma katika shule ya sekondari ya Feza Girls iliyoko Kawe jijini Dar es Salaam, na alipata alama ‘B’ katika somo la Kiswahili.
Hata hivyo, Congcong amefunikwa na Butongwa Charles Shija, aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa akitoka katika shule ya Canossa iliyoko jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari nyumbani kwao jijini Dar es Salaam, Butongwa alieleza kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii wakati wote bila kujali kama sio kipindi cha mitihani, tofauti na wanavyofanya wanafunzi wengi.
Alisema kuwa mtindo huo wa kusoma ulimfanya kuwa na uelewa mpana wa masomo yake na kuwa tayari wakati wote kujibu maswali ya mtihani kwa ufasaha muda wowote.
Alisema kuwa ndoto yake ni kusoma katika Chuo Kikuu cha Harvard, Chuo ambacho ni kikubwa na chenye heshima duniani.
“Nilipoanza shule, niliwaambia wazazi wangu kuwa ndoto yangu ni kusoma Chuo Kikuu Cha Harvard. Walinieleza kuwa sio jambo rahisi, lakini nilisema hata kama sio Harvard basi moja kati ya vyuo vikuu 10 vikubwa zaidi duniani,” alisema Butongwa.
Alisisitiza kuwa bado ndoto yake ni kusoma katika chuo kikuu hicho na nia yake ni kusomea udaktari ili awe msaada mkubwa kwa taifa katika sekta ya afya.
Akitangaza matokeo ya kidato cha nne, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Charles Msonde alisema kuwa watahiniwa wa shule, waliofaulu ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 ya waliofanya mtihani, wasichana wakiwa 11,125 (64.84) na wavulana wakiwa 124,871 (71.09). Ufaulu huo umeshuka kwa asilimia 1.85, ukilinganishwa na ufaulu wa mwka 2014.