Serikali imesema kuwa mtazamo yakinifu wa Rais Dkt. John Magufuli katika usimamizi na ufuatiliaji wa sekta ya madini, umewezesha ongezeko maradufu la makusanyo ya mapato ya sekta hiyo kutoka Tsh. Bilioni 210 mwaka 2015/16 hadi kufikia Tsh Bilioni 302 kwa mwaka 2018/19 na kuifanya Tanzania kuzidi kujijenga Kiuchumi.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kisayansi na itahakikisha rasilimali za nchi zinaendelea kulindwa ili ziweze kuleta manufaa kwa Watanzania wote.
Amesema kuwa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Novemba 2015, ilifanya mageuzi mbalimbali katika usimamizi na ufuatiliaji wa rasilimali za madini, kwani huko nyuma Serikali ilikuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha na kuamua kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
“Tulipofanya marekebisho katika sheria yetu ya madini mwaka 2017, matokeo tumeanza kuyaona kwani tumedhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato yetu na kuanza kusimamia kwa umakini mkubwa utoroshaji mkubwa wa madini ambapo ilisababisha Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mapato,” amesema Dkt. Abbasi.
Aidha, kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kuanzishwa kwa masoko ya madini ambayo ni utekelezaji wa sheria ya madini ya mwaka 2017, hadi sasa kuna jumla ya masoko 24 ambayo yamekuwa yakithibiti ubora, thamani na takwimu za madini nchini, ambapo soko la kwanza lilianzishwa Mkoani Geita, mwezi Machi mwaka huu.
Pia ameongeza kuwa Takwimu za jumla za uzalishaji wa dhahabu katika kipindi cha miezi miwili mkoani Geita kuanzia mwezi Machi hadi Mei, mwaka huu zinaonyesha kuwa uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia kilo 312.65 za dhahabu ukilinganisha na uzalishaji wa dhahabu kilo 259.12 zilizokuwa zikizalishwa kabla ya masoko hayo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa eneo lingine la mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini ni pamoja na maamuzi iliyochukua ya kujenga ukuta kuzunguka eneo la wachimbaji wa Madini ya Tanzanite Mkoani Manyara ambao Serikali iliweka mifumo ya masoko na ukaguzi, na hivyo kuchangia ongezeko la mapato ya wachimbaji wadogo na Serikali kwa ujumla.