Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC limetoa pongezi kwa wachezaji wake kwa kufanikisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, leo Jumatatu (Machi 07).
Simba SC ilikua mwenyeji katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam majira ya saa moja usiku.
Akizungumza kwa niaba ya Benchi la Ufundi la klabu hiyo, Kocha Msaidizi Selemani Matola amesema wachezaji wameonesha kupambana na kufanikiwa kupata matokeo.
Amesema kujituma na kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi kwa wachezaji wao, imewasaidia kufikia lengo la kuwafurahisha mashabiki na wanachama wanaoendelea kuiombea timu yao kila kukicha.
“Tunawapongeza wachezaji wetu kwa kufanikisha hili, ilikua kazi kubwa na isiyo rahisi kuifunga Dodoma Jiji, wapinzani wetu walikuja na mbinu ya kutubana na kushambulia kwa kushtukiza na ndio maana katika kipindi cha kwanza walitupa tabu.”
“Kipindi cha pili tuliingia kwa nguvu na kuwalazimisha kufanya makosa ili tuwafunge, na kweli ilikua hivyo kwa tukio la penati na mazingira ya upatikanaji wa bao la pili.” amesema Matola
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo yamepachikwa wavuni na Clatous Chama kwa mkwaju wa penati na Meddie Kagere.
Ushindi huo unaiwezesha Simba SC kufikisha alama 37 zinazoiweka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakitanguliwa na Young Africans iliyo kileleni kwa alama 45.