Benchi la ufundi la klabu ya Simba limejinasibu kuwa chagizo kubwa katika usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Uganda, Khamis Kiiza Diego ambaye muda si mrefu atajiunga na wachezaji wa klabu hiyo ambao tayari wameshaanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Kocha msaidizi wa klabu ya Simba Suleyman Matola amesema mipango ya kusajiliwa kwa Kiiza ilipendekezwa na benchi lao la ufundi kufuatia hitaji mshambuliaji ambalo anaamini limepatiwa ufumbuzi, baada ya kuonekana ulikua na mapungufu msimu uliopita.

Matola amesema ujio wa Mshambuliaji huyo ambaye alitemwa na klabu ya Dar es salaam Young Africans wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka 2014, utaongeza chachu kwa wachezaji wenzake ambao tayari wameshaanza mazoezi ya Gym.

“Kama tasajiliwa Kiiza itakua ni vizuri sana kwetu, kwa sababu sisi tulipendekeza usajili wa mchezaji anayecheza nafasi ya ushambuliaji baada ya kuona mapungufu msimu uliopita.” Alisema Matola

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema wako katika hatua za mwisho kumsajili mshambuliaji huyo.

Kwa upande wa mshambuliaji huyo ambaye alikua mpambe wa bwana harusi wakati wa sherehe ya ndoa ya Emmanuel Okwi mwishoni mwa juma lililopita, amesema wakala wake amefikia hatua nzuri na Simba, hivyo wakati wowote anaweza kusaini mkataba.

“Ni kweli wakala wangu amekuwa akizungumza na Simba, ameniambia wamefikia hatua nzuri, wakimalizana kila kitu, nitasaini Simba”. Amesema Kiiza.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amesema kama atajiunga na Simba itakuwa furaha kwake kucheza timu moja na rafiki yake Emmanuel Okwi.

“Okwi ni rafiki yangu wa siku nyingi toka tukiwa shule, tulicheza pamoja toka tukiwa wadogo, ndio maana uliona hata kwenye harusi yake mimi nilikuwa msindikizaji wake, nitafurahi kucheza naye Simba”. Ameongeza Kiiza.

Uwanja Wa Millennium Kuwa Mwenyeji Fainali Mabingwa Ulaya
Nike yazindua mipira ya Uingereza, Hispania na Italia Msimu Wa 2015-16