Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Seleman Matola amesema kesho Jumamosi (April 03) itawalazimu kusaka ushindi dhidi ya AS Vita Club, ili kufikia lengo la kufuzu hatua ya Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Matola ametangaza uhakika huo alipozungumza na waandishi wa habari leo mchana jijini Dar es salaam katika mkutano maalum ambao ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mchezo huo ambao utaanza saa 10:00 jioni.
Kocha huyo mzawa amesema Simba SC imejipanga kupata matokeo dhidi ya AS Vita Club, licha ya kuhitaji alama moja ili kujihakikshia kutinga hatua ya Robo Fainali.
“Kesho ni lazima tupate matokeo ili tusonge mbele, tumejipanga kupata matokeo. Tunamshukuru Mungu hakuna mchezaji ambaye tutamkosa, wote wapo kambini na hilo linatupa mwanga kuwa tunaweza kufanya vizuri.” Amesema Matola.
Naye nahodha na mshambuliaji wa Simba SC John Raphael Bocco amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kwa kusisitiza kuwa wamejipanga kupambana na kupata matokeo dhidi ya AS Vita Club.
“Kwa upande wetu kama wachezaji tuko vizuri, tuna ari nzuri ya kuweza kupambana ili kufikia malengo ya timu yetu. Tumefanya maandalizi mazuri na tunaamini Mungu atatusaidia na tutafuzu hatua ya robo fainali.
“Tuna wachezaji wenye uzoefu mkubwa na wanaoelewa kwanini wapo kwenye klabu. Tuko tayari.” Amesema John Bocco.
AS Vita Club yenye alama nne, inahitaji matokeo ya ushindi tu katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba ili iweke hai matumaini yake ya kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Barani Afrika msimu huu 2020/21.
Simba SC inaongoza msimamo wa Kundi A kwa kufikisha alama 10, ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama 7, AS Vita inashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 4 na AlMerrikh wanaburuza mkia kwa kupata alama moja kwenye michezo minne waliocheza.