Baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na uongozi wa Lipuli FC, kocha Suleyman Matola ametangaza hadharani mipango yake ya usajili kwa kusema itazingatia sana vijana wenye vipaji.
Matola ambaye alikua kimya tangu alipozimiwa ndoto zake za kukinoa kikosi cha Geita Gold Sports baada ya kuibuka kwa tuhuma za upangaji wa matokeo, amesema anaamini katika soka la vijana ndipo penye ushindani wa kweli.
“Ninaamini katika soka la vijana, nimekua ninafanya hivyo tangu nilipoanza kazi ya ukufunzi wa soka, kwa hiyo sina wasiwasi na usajili nitakaoufanya ambao utazingatia sana vijana.” Amesema Matola
“Tanzania kuna wachezjai wengi wenye uwezo wa kucheza soka lakini wamekua hawaaminiwi, binafsi nataka kuonyesha hilo linawezekana, endapo vijana hawa watapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara.”
Kocha Suleyman Matola.
Hata hivyo Matola amesema ataheshimu na kuifanyia kazi ripoti iliyoachwa na kocha aliyemtangulia, huku akisistiza kuendelea kufanya kazi na wachezaji wa Lipuli FC waliopambana kuipandisha daraja klabu ya mkoani Iringa.
“Natambua kuna ripoti ya kocha aliyenitangulia, Nitakapozungumza na viongozi wangu kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kupanga mikakati ya kazi nitakayoifanya, nitaiomba na kuipitia kwanza, naelewa kuna jambo nitalipata katika hiyo ripoti.
“Pia kuna baadhi ya wachezaji watakua wamependekezwa kuachwa na wengine kuendelea na timu, hivyo nitajadiliana na viongozi wangu kupitia hiyo ripoti ili kujua nani anaondoka na nani anabaki ili kutoa nafasi ya wengine kusajiliwa kwa ajili ya kukiboresha kikosi.” Aliongeza Matola.
Lipuli ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda daraja msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na Njombe Mji ya Mkoani Njombe na Singida United baada ya kufanya vyema Ligi Daraja la Kwanza.