Kocha Msaidizi wa Simba SC Seleman Matola amevunja ukimya na kukanusha tuhuma zilizowahi kuelekezwa kwake kutoka kwa Baadhi ya Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo ya Msimbazi.
Matola amekanusha tuhuma hizo saa chache kabla ya kuondoka klabuni hapo kwa ajili ya kwenda kuanza Kozi ya Ukocha ngazi ya Diploma A ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Matola amesema hakuwahi na wala hatawahi kuihujumu Simba SC na wakati wote akiwa kazini alifanya kazi kwa weledi mkubwa kwa kuheshimu maagizo kutoka kwa Mkuu wake ‘Kocha Mkuu’.
“Hakuna mtu ambaye anafurahia tuhuma zinazoelekezwa kwake ambazo sio za kweli, kwa kweli hilo likikufika linaumiza sana, kwa sababu unatuhumiwa kwa jambo ambalo hujalifanya na wala hufikirii kulifanya.”
“Kwa mtu anayejua kazi ya mpira hawezi kufanya kitu kama hicho, kwa sababu kwenye mpira Bosi ni Kocha Mkuu, kwa hiyo kinachoamuliwa na ukaagizwa unapaswa kukifanya, hivyo sijawahi na wala sitawahi kuihujumu Simba SC.” amesema Matola
Matola amekua Muhimili Mkubwa Simba SC tangu alipokua mchezaji kama Nahodha na baadae Kocha Mkuu wa kikosi cha Vijana kisha alipandishwa kuwa Kocha Msaidizi wa Kikosi cha Wakubwa huku akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu kwa vipindi tofauti.