Beki wa kati wa klabu bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich Mats Hummels, hatokua sehemu ya kikosi cha mabingwa watetezi wa dunia katika mchezo wa leo wa kundi F dhidi ya Sweden.
Beki huyo ataukosa mchezo huo, kufuatia maumivu ya shingo aliyoyapata akiwa mzoezini na wenzake, na tayari imethibitika huenda ikamchukua muda wa siku kadhaa kabla ya kurejea tena uwanjani.
Kocha Joachim Low ameonyesha masikitiko ya kumkosa beki huyo katika mchezo dhidi ya Sweden, ambao utaanza mishale ya saa tatu usiku kwa saa za Afrika mashariki.
Low amesema Hummels alikua na umuhimu mkubwa katika mpambano huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani, kutokana na umahiri wake.
Kocha huyo amesema pamoja na kutarajia kumkosa Hummels, bado anaamini siku kadhaa zijazo, beki huyo atakua sawa kwa ajili ya kuendeleza mapambano ya kutetea ubingwa wao wa dunia huko nchini Urusi.
“Hummels hatokuwa sehemu ya kikosi cha Ujerumani katika mchezo dhidi ya Sweden, aliumia shingo akiwa katika maandalizi ya mchezo huu, ambao kwetu una umuhimu mkubwa sana,” amesema Low.
“Nilihitaji kumtumia katika mchezo huu, lakini sina budi kumpumzisha kutokana na hali yake, japo ninaamini atarejea tena kuendelea na mapambano ya michezo itakayotukabili baada ya kupambana na Sweden.”
Hata hivyo Low amesema kikosi chake kwa ujumla kipo tayari kwa mchezo wa leo, na ana uhakika watafanya vizuri, baada ya kutambua makosa waliyoyafanya kwenye mchezo wa kwanza wa kundi F, ambao ulishuhudia wakipoteza dhidi ya Mexico kwa kukubali kufungwa bao moja.
Wakati huo huo Hummels amewahamasisha wachezaji wenzake kwa kuwambia wanastahili kupambana vilivyo katika mtanange wa leo, ili kuweka matumaini ya kusonga mbele.
Hummels amefanya kazi hiyo kambini, na baadae kuthibitisha katika ukurasa wake mtandao wa Twitter kwa kuanzindika “Bado tuna matumaini kupitia mchezo wetu wa kesho (leo), usikose kuufuatilia mchezo huo ambao utakua na umuhimu mkubwa.”
Kikosi cha Ujerumani kitahitaji kushinda dhidi ya Sweden ili kufufua matumaini ya kusonga mbele katika fainali za mwaka huu, na kama kitapoteza kitatupwa nje ya michuano hiyo inayoendelea nchini Urusi, na kuutema ubingwa rasmi.