Shirikisho la soka nchini (TFF), limemwondoa Mwamuzi Hussein Athuman kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.
Mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi alichezesha mchezo namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Young Africans ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Kadhalika Young Africans imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yao kutoingia vyumbani, na pia kutumia mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi Ngole Mwangole: Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya amepewa barua ya onyo kali na kumtaka aongeze umakini wakati akichezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kubainika kukataa bao lililoonekana kutokuwa na mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Licha ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa Bw. Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu uliopita (2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya uamuzi uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.
Mechi namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar, Godfrey Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi baada ya mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la ufundi la timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti kadhia hiyo.
Mechi namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.
Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi.
Hivyo, Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. Kama marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.
Mechi namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.
Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.
Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.
Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.
Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.
Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.
Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.
Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili kupoteza muda.
Mechi namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi Daraja la Pili.
Malalamiko mbalimbali
Malalamiko ya klabu za Mwadui FC na Polisi Morogoro kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji wa Stand United, Kheri Mohamed Khalifa na wachezaji wawili wa Njombe Mji kucheza mechi bila leseni yamepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Pia maombi ya klabu ya Singida United kuhusu kubadilishiwa Mwamuzi kwenye mechi yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi, wakati maombi ya Alliance Schools, Friends Rangers FC, The Mighty Elephant na Kariakoo FC yanayohusu uendeshaji yanashughulikiwa na Sekretarieti ya TPLB.
Kuhusu JKT Ruvu
Katika mengineyo, Kamati ilipitia maombi ya timu ya JKT Ruvu Stars FC kubadilisha uwanja wake wa nyumbani kutoka Mabatini mkoani Pwani hadi Mkwakwani mkoani Tanga kutokana na wachezaji wake 12 wa kikosi cha kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi mkoani Tanga.
Ombi hilo limekubaliwa. Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(6) ya Ligi Kuu, TFF/TPLB zina mamlaka ya mwisho kuhamisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona zinafaa na kwa wakati husika.
Kuhusu Mchezaji Venance Ludovic
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajiwa kukaa wiki ijayo kusikiliza malalamiko dhidi ya usajili wa wachezaji mbalimbali akiwemo mchezaji Venance Joseph Ludovic.