Umoja wa mataifa umeripoti kuwa kila mwaka wanawake 300,000 hufariki dunia kutokana na Saratani ya Mlango wa Kizazi huku ikiaminika kuwa Saratani hiyo inaweza kuwa aina moja ya saratani ya kwanza kutokomezwa ikiwa asilimia 90 ya wanawake watapata chanjo.
Akizungumza na Dar24 Media, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean road, Dkt. Julius Mwaiselage amesema katika kupambana na Saratani hiyo, Taasisi ya Ocean road imeanza kutoa chanjo tangu mwaka 2018 katika shule mbalimbali.
Mwaiselage amesema zoezi hilo linafuatiliwa kwa ukaribu kuhakikisha watoto wa kike wanapata chanjo hiyo bila kukosa huku akieleza kuwa mwitikio wa chanjo ni zaidi ya asilimia 80.
Amesema endapo chanjo itafuatiliwa kwa ukaribu, baada ya miaka 15 na kuendelea kunaweza kukawa na upungufu wa wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa asilimia 90 .
Aidha amewaasa vijana kuacha ngono zembe na wanawake kupima mara kwa mara saratani hiyo kwani matibabu yake ni bure nchini, ambapo kuna vituo zaidi ya 700 vinavyopima saratani hiyo.
Kwa upande wa Tanzania inakadiriwa wagonjwa wanaojitokeza kila mwaka wenye saratani ni 7000 na wanaofariki kwa ugonjwa huo ni 4200.
Mwezi Januari hutumiwa na Umoja wa Mataifa kama mwezi wa kuongeza uelewa wa saratani ya mlango wa kizazi ambayo huwathiri wanawake.