Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya bado lipo nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa kwani kuna baadhi ya maeneo nchini yanahusika na kilimo cha bangi katika safu za milima na misituni.
Rais Samia ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere na kuzima mbio za mwenge yaliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita.
Rais Samia ameongeza kuwa Kilimo hiki hakina baraka za mwenyezi Mungu, kwa kuwa mazao ya kilimo hiki yakitumika vibaya yanachangia kuharibu afya ya akili ya vijana wetu na wataalamu wanasema sababu kubwa za magonjwa ya akili kuongezeka nchini ni matumizi ya madawa ya kulevya na Bangi
“Niwasihi vijana wa Tanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa matumizi haya ya dawa za kulevya na magonjwa kama Tb, Ukimwi na UVIKO 19 kwani hali ya maambukizi ya magonjwa bado ipo juu na niwaombe watanzania waende wakachanje kwani bila afya bora hatutaweza kuimarisha uchumi wa nchi yetu”
Amesema kwa siku 150 za mbio za mwenge vijana waliohusika kukimbiza Mwenge wamefanya kazi kubwa kuyasemea yote na kumulika maovu katika jamii ikiwemo uzembe, ubadhirifu, wizi, kuvuta bangi na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo yote hayo yanaleta vikwazo na kupunguza nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana.
Rais Samia katika hatua nyingine amesema Serikali itaendeleza kuenzi na kudumisha mambo yote mazuri yaliyoachwa na baba wa taifa kwani kuendeleza falsafa na maono na mema yake kunahitaji hekima na busara ya kutosha.
“Mwalimu Nyerere alikua kiongozi bora asiependa ubaguzi wa aina yoyote, aliwajali wanyonge ambao walihitaji kukombolewa katika mazingira yasiyo ya haki kutoka kwa wengine, hakika alikua na Moyo Rahimu, aliwaelekeza watanzania kujenga mshikamano na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili waweze kuishi wakiwa huru katika nchi yao” amesema Rais Samia.
Serikali iliamua kuunganisha matukio matatu ya siku ya kuzima Mwenge, kumbukumbu ya mwalimu Nyerere na wiki ya vijana ili kuwapa fursa watanzania wa kizazi cha leo na vizazi vijavyo kukuza shughuli za kuenzi kukuza historian a kukumbushana falsafa zinazoongoza nchi ya Tanzania.
Maadhimisho haya ya siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere na mbio za mwenge yamekua na kauli mbiu inayosema “Tehama ni msingi wa taifa endelevu itumiwe kwa usahihi na uwajibikaji”