Matumizi ya zana za kijeshi duniani yameongezeka na kufikia takribani dola trilioni 2, licha ya uwepo wa janga la virusi vya corona.
Mtafiti wa Taasisi ya Kimataifa inayohusika na utafiti wa masuala ya amani SIPRI), anayehusika na silaha na programu ya matumizi ya kijeshi, Diego Lopes da Silva amesema janga la virusi vya corona halikuwa na athari zozote katika matumzi ya zana za kijeshi kwa mwaka 2020.
Mataifa ambayo yanaongoza katika matumizi makubwa ya silaha ni Marekani, China, India, Urusi na Uingereza ambayo kwa pamoja hayo yanafanya jumla ya asilimia 62 ya matumizi ya silaha duniani, lakini kwa namna ya kipekee kiwango hicho kwa China kimekuwa kikiongezeka kwa takribani mwaka wa 26 kwa mfululizo.
Aidha Marekani ambayo inatajwa kuwa kinara wa kutumia fedha nyingi katika sekta yake ya ulinzi, kwa mujibu wa SIPRI kwa mwaka 2020, matumizi yake ya kijeshi yanakadiriwa kufikia dola bilioni 778 likiwa ni ongezeko la asilimia 4.4 ikilinganishwa na mwaka 2019.
Kwa hatua hiyo, Marekani inahesabiwa kutumia asilimia 39, ya jumla ya asilima zote za matumizi ya kijeshi duniani.
Hili pia ni ongezeko la mara ya tatu mfululizo, baada ya miaka mengine saba ya jitihada za kupunguza matumizi hayo.