Shirika la Afya ulimwengu – WHO, kanda ya Afrika limeipongeza nchi ya Mauritius kwa kutambuliwa leo huko Geneva Uswis kwa juhudi zake za kupambana na athari za tumbaku kwa umma baada ya kufanikiwa kupunguza kwa asilimia 25 maambukizi ya uvutaji sigara kati ya watu wazima kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1992 mpaka 2021.
Waziri Mkuu wanchi hiyo, Pravind Kumar Jugnauth ametaja utashi wa kisiasa kuwa ndiyo siri kubwa ya mafanikio yao na kusema dhamira yao imewapatia maendeleo katika sera za kudhibiti tumbaku nchini humo.
Ripoti iliyotolewa jijini Geneva nchini Uswisi na Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghabreyesus imesema Mauritius inaungana na nchi za Brazil, Uturuki na Uholanzi katika mafanikio ya kukomesa uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma na ikiwa mwanzilishi wa sheria ya kudhibiti tumbaku.
Nchi hiyo, ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kuridhia Mkataba wa Mfumo wa WHO wa Kudhibiti Tumbaku mwaka 2004, na pia ni mojawapo ya nchi za kwanza kuweka maonyo ya picha na maandishi kwenye vifungashio vya tumbaku mwaka 2008.