Kiungo Mkabaji wa Young Africans Zawadi Mauya amefunguka namna alivyofunga bao lililoipa ushindi timu yake dhidi ya Simba SC, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mauya ambaye alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa Msimu huu 2020/21 akitokea Kagera Sugar amesema hakua na uhakika kama mpira alioupiga ungeingia langoni mwa Simba SC, zaidi ya kutimiza jukumu la kupiga kutokana na nafasi aliokuwepo.

Amesema alipoona mpira umekuja mbele yake, na kama ilivyo ada kwa mchezaji hujaribu pale anapoona nafasi, na alipojaribu kufanya hivyo alifanikiwa kuipatia bao timu yake ambayo ilikua haipewi nafasi kubwa ya kuondoka na alama tatu.

“Tulicheza mchezo mzuri. Lile goli sikupanga, ila ilitokea tu. Ulikuja mpira uliookolewa ukawa unazagaazagaa pale na mimi niko karibu nikaukimbilia na kuupiga, lakini kwa sababu tulikuwa na jambo letu, ngoma ikaenda hadi mwisho,” amesema Mauya

Mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC, ulikua wa kwanza kwa Zawadi Mauya kucheza na kubahatika kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuifunga timu ambayo ni mpinzani mkubwa wa Young Africans kwa Tanzania.

Ushindi wa Young Africans dhidi ya Simba SC, umeifanya klabu hiyo kufikisha alama 70, ambazo zinaendelea kuwaweka kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2020/21.

Simba SC wanaendelea kuwa na alama 73, zinazowaweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikisaliwa na michezo minne dhidi ya KMC FC, Coastal Union, Azam FC na Namungo FC.

Mzee Mpili: Simba SC atapigwa Kigoma
Messi aiweka njia panda FC Barcelona