Siku chache baada ya rapa XXXTentacion kuuawa kwa kupigwa risasi, ripoti zinaonesha kuwa mauzo ya nyimbo na albam yake yamepanda kwa kasi kwa asilimia 1,600 kupitia mitandao ya Amazon Music na iTunes.
Jumanne, siku moja baada ya kifo chake, Billboard iliripoti kuwa mauzo ya muziki wa rapa X ambaye alikuwa ‘rapa mtata’ kutoka Florida yamepanda kutoka nakala 2,000 zilizouzwa Juni 17 hadi nakala 33,000 zilizouzwa Juni 18.
Kutokana na kupanda kwa mauzo haya, Billboard wamesema kuwa wanatarajia kuirudisha albam ya rapa huyo ‘?’ kwenye Billboard 200 wiki ijayo.
Kwa mujibu wa XXL, kwa ujumla ndani ya saa 24 mauzo ya nyimbo zake hususan ‘Sad’ ambao uko kwenye albam ya ‘?’ imepakuliwa na kusikilizwa mara nyingi zaidi na kuchangia mauzo hayo kufikia asilimia 1,600 ya ilivyokuwa siku moja kabla.
‘?’ iliyotoka Machi mwaka huu ilishika nafasi ya kwanza kwenye chati hizo ikiwa ni mafanikio ya juu zaidi baada ya ile ya ‘17’ iliyotoka Septemba mwaka jana kushika nafasi ya pili kwenye chati hizo.
Rapa X alikuwa rapa aliyeingia kwa kishindo kwenye kiwanda cha muziki, hadi kufikia hatua kuanza kulinganishwa na Kendrick Lamar ambaye bado anatajwa kuwa huenda ndiye rapa mkali zaidi aliyeibuka kwenye kizazi kipya, ukiacha nguli wa muziki huo.
- Makamba azua gumzo na ‘kanuni’ za kutumia lifti za majengo marefu
- Mwanamke akutwa ndani ya tumbo la Chatu
Kendrick Lamar alikuwa mstari wa mbele pia kumuunga mkono rapa XXXTentacion aweze kupiga hatua zaidi kwenye muziki wake.
Rapa huyo aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatatu wiki hii na watu wawili wenye bunduki, katika tukio linalotajwa kuwa lilikuwa la ujambazi.