Wakati jicho la dunia ya siasa za Penisula ya Korea likiangazia mkutano mkubwa na wa aina yake kati ya viongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un na wa Korea Kusini, Moon Jae-in kwa mara ya kwanza katika historia baada ya vita ya mwaka 1953, jicho la wadau wa mitindo duniani limemuona na kumtunuku taji mke wa Kim Jong-un.

Ri Sol-ju, mwanamke mrembo mwenye umri wa miaka 29 ameingia kwenye rekodi kubwa ya mitindo kwa mavazi aliyovaa ndani ya siku mbili na kuonekana hadharani katika mkutano huo ambapo amekuwa bega kwa bega na mke wa rais wa Korea Kusini.

Mpangilio wa vazi lake la suti ya aina yake, imewafanya wachambuzi wa masuala ya mitindo duniani kumvika taji la ‘kielelezo cha mtindo bora wa mavazi katika Penisula ya Korea’.

Jarida la Korea Herald limeripoti kuwa tangu aonekane hadharani, Ri Sol-ju amekuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wengi ambao wameanza kuvaa mavazi kama yake na kuyafanya kuwa mtindo rasmi wa eneo hilo.

Mke wa Kim Jong Un (kushoto) akiwa na mumewe, wakiongozana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in akiwa na mkewe Kim Jung-sook

Uchaguzi wa mavazi yake uliowekwa wazi na kujadiliwa zaidi Ijumaa iliyopita kwenye kijiji cha Panmunjom katika mpaka wa nchi hizo, imelazimu vyombo vya habari hadi vya Magharibi kwa mara ya kwanza kuripoti kitu kinachoonesha mapenzi na mvuto kuhusu Korea Kaskazini. Awali habari za makombora ya kinyuklia na ukatili zilitawala kama picha ya nchi hiyo.

Mwanamke huyo aliambatana na mke wa rais wa Korea Kusini wakiwa wameshikana mikono, nyuma ya viongozi hao wa nchi hizo mbili waliokuwa wametangulia kuashiria amani na mshikamano.

Jina la mwanamke huyo ambaye ni ubavu wa kiongozi aliyewahi kutajwa kuwa na uamuzi wa hatari dhidi ya watumishi wake wanaomkosea pamoja na mataifa ya Magharibi, limekuwa jina linalouza mtindo mpya wa mavazi.

 

Mohamed Salah Ghaly mchezaji bora F.W.A
Arsenal wana mpango na Zeljko Buvac?