Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewahakikishia Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kuendeleza Mageuzi ya Kimkakati yanayoendelea katika Sekta ya Madini na kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuikuza Sekta ya Madini.
Ameyasema hayo Septemba 4, 2023 wakati akizungumza kwa mara ya kwanza katika Ofisi za Wizara ya Madini na kupokelewa na Viongozi wakuu wa wizara na taasisi zake jijini Dodoma.
“Niwahakikishie kuwa nakuja kufanya kazi na nitaendeleza yale yaliyofanywa na mtangulizi wangu aliyepita Dkt. Doto Biteko kwa ushirikiano mkubwa,” amesema Waziri Mavunde.
Amesisitiza kuwa, kutokana na mchango wake katika Pato la Taifa, Sekta ya Madini kwa sasa imepiga hatua kubwa kwenye mchango wake na mabadiliko yaliyotokea katika sekta yameondoa migogoro kwa wachimbaji wa madini nchini kwa kuendelea kufanya shughuli zao kwa usalama.
Katika hatua nyingine, ameahidi kushirikiana na Watumishi wote wa Wizara ya Madini ili kuendelea kuleta tija katika sekta hiyo yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.
Waziri Mavunde anatarajia kupokea taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kuongeza kwamba amepanga kuzifikia taasisi nyingine wiki hii ili kuona namna zinavyotekeleza shughuli zake.
Pia, amesema atayaishi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Maagizo na Miongozo ili hatimaye Sekta ya Madini kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameahidi Waziri kumpatia ushirikiano wa kutosha ili lengo la Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa liweze kufikia ifikapo Mwaka 2025.
Wengine walioshiriki katika mapokezi hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Idara na Vitengo na Watumishi wa wizara.