Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde amesema kuwa Taifa lenye maadili ndilo linaloishi na watu wanapokosa maadili Taifa linakufa.
Mavunde amesema hayo wakati akiwahutubia vijana zaidi 3,500 wanaosoma vyuo vya elimu ya juu vya mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mkesha wa kusifu na kuabudu (Campus Night 2017) kwenye ukumbi wa Chimwaga, mjini Dodoma.
“Naendelea kuiona Tanzania yenye ustawi mkubwa sana kama tutakuwa na vijana wenye kumjua Mungu, wenye hofu ya Mungu na wenye kufuata maadili mema kwani kukosa maadili kunaua Taifa,” alisema Naibu Waziri huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Aliwataka vijana hao watambue kuwa wameletwa vyuoni kusoma na siyo kujihusisha na mambo ambayo ni kinyume na maadili. “Katika maisha lazima utambue njia yako, usipoijua utapata shida tu. Ukiifahamu njia yako ni lazima unaitunza hadi ikufikishe mwisho,” aliongeza.
Akitoa mfano, Naibu Waziri Mavunde aliwaeleza wanavyuo kwamba hakuna jambo baya kama mtu kufikia hatua ya kuingia chuo kikuu au chuo kingine cha elimu ya juu lakini asijue anapaswa kufanya nini.
“Hakuna jambo baya kama hivi sasa uko chuo kikuu lakini hujajua unataka kufanya nini maishani mwako. Ni sawa na kufanya biashara ya kununua mablanketi na kwenda kuyauza Dar es Salaam ambako kuna joto wakati wote au kuamua kufanya biashara ya ice cream katika maeneo ya baridi kama vile Mafinga,” alisema.