Katibu wa Chama cha Wanasheria nchini Chad, Koulmem Nadjiro amesema mawakili wanatarajia kukata rufaa dhidi ya mashtaka ya waandamanaji 262 kati ya 401 waliokamatwa Oktoba 25, 2022 na kuhukumiwa.
Nadjiro amesema, Waandamanaji hao wamehukumiwa na wengine wameachiwa lakini hiyo haimaanishi kuwa utaratibu ulifuatwa kitu ambacho kinatoa nafasi kwa mawakili kukata rufaa ili kuona namna ya kuwaondoa kifungoni wote waliohukumiwa bila haki.
Amesema, “Tunachokikosoa sisi watetezi wa haki za binadamu kwa vile Mahakama imetenda kinyume na utaratibu ambao umekuwa ukifuatwa kisheria, kwasababu upo upendeleo unaopoka haki na hukumu zenye usawa.
Katibu huyo wa Chama cha Wanasheria wa Chad ameongeza kuwa, “Kwa hivyo mawakili watalazimika kukata rufaa ili kupata haki. Natumai majaji wa rufaa watafuata sheria.”
Takriban watu 50, ikiwa ni pamoja na wanachama 10 wa vikosi vya usalama, walikufa wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji katika mji mkuu wa N’Djamena, na miji mingine kadhaa mnamo Oktoba 20, 2022.
Maandamano hayo, yalikuwa yameitishwa kuashiria tarehe ambayo jeshi tawala la Chad liliahidi awali kuachia madaraka, muda ambao sasa umeongezwa na kuwa miaka miwili huku Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno akiwashutumu waandamanaji kwa “maasi” na kujaribu kufanya mapinduzi.