JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 8 Juni, 2022 aliendelea kufanya usaili kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa wanafunzi 321 waliofaulu mitihani yao katika Shule ya Sheria kwa vitendo na Baraza la Elimu ya Sheria wanaoomba kuorodheshwa kwenye daftari la Mawakili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa kwenye moja ya matukio ya shughuli zake za kila siku za kiofisi.
Waombaji hao kutoka Kanda za Dodoma na Tabora walifika mbele ya Jaji Mkuu kwa njia ya mtandao kupitia miundombinu iliyowekwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora na Kituo Jumuishi cha utoaji haki Dodoma na kufanya usahili, hivyo kuokoa muda, gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano, takribani waombaji 152 kutoka Dar es Salaam, Mtwara, Tanga Dodoma na Tabora tayari wamekwishafika mbele ya Jaji Mkuu kufanyiwa usahili huo. Zoezi hilo linaendealea katika vituo vingine vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda za Mwanza, Bukoba, Arusha na Mbeya ambapo waombaji wengine takribani 160 kutoka maeneo ya jirani watafanyiwa usahili huo unaoendelea nchi zima kulingana na Kada hizo.
Mhe. Kirekiano amesema kwa sasa zoezi limeenda vizuri kwa kuzingatia kwamba nchi yetu ni kubwa uwepo wa vifaa vya TEHAMA katika kila kituo cha Mahakama Kuu Kanda husika vimesaidia kufanikisha zoezi hilo. Aidha, alimshukuru Jaji Mkuu kwa kuruhusu zoezi hilo kufanyika kwa njia ya TEHAMA.
Naye mmoja wa washiriki wa usahili huo, Wakili mtarajiwa Bi. Mwanabibi Kalambo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa juhudi zake za kuhimiza na kukuza matumiza ya TEHAMA katika kutekeleza majukumu yake.
Picha ya pamoja ya Watahiniwa wa usaili wanaoomba kuorodheshwa kwenye daftari la Mawakili kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda za Dodoma ikiwa ni miongoni wa wanafunzi 321 wanaoendelea kushiriki zoezi hilo kwa nchi zima.(Picha na Innocent Kansha-Mahakama).
“Nadhani ni jambo zuri sana kwa Mahakama kukuza matumizi haya ya mfumo wa mawasiliano, nawaza kama nigesafiri kutoka Dodoma hadi Dar es salaam ningetumia gharama kubwa na muda ungekuwa mrefu na washiriki kwa vile tungekuwa wengi sehemu moja. Matumizi ya TEHAMA yamesaidia kuokoa muda, gharama na kuondoa usumbufu kwani mahojiano yalichukua muda mfupi sana na mawasiliano yalikuwa ya kiwango bora,”alisema Mwanabibi.
Sherehe ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili hao wapya, kula kiapo cha uadilifu na kuorodheshwa kwenye daftari la Mawakili inatarajiwa kufanyika Julai 8, 2022 jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.