Mkutano wa kibiashara kati ya Afrika na Marekani umeanza nchini Afrika Kusini, huku jiji la Pretoria na Washington wakirekebisha uhusiano wao baada ya mzozo kuhusu shutuma kwamba Afrika Kusini inajihusisha na Russia.
Mawaziri kutoka nchi zipatazo 40 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinazonufaika na Sheria ya Ukuaji na Fursa kwa Afrika – AGOA, watafanya mazungumzo ya siku tatu na wajumbe kutoka Marekani huko Johannesburg.
Naibu Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika, Joy Basu amesema uchaguzi wa Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika kila mwaka, umekuwa ishara ya kujitolea kwetu kwenye uhusiano wetu wa pande mbili.
Bunge la Marekani mwaka 2000 liliidhinisha AGOA kuwa ndiyo msingi wa sera ya uchumi na biashara ya Marekani katika bara la Afrika, huku mkataba huo ukitoa nafasi kwa nchi ambazo zinakidhi vigezo vya kidemokrasia vinavyo tathminiwa kila mwaka.