Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha Mawaziri watatu aliowateua Machi 3, mwaka huu, kushika nyadhifa katika Wizara tofauti za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mawaziri walioapishwa ni Dkt. Sada Mkuya Salum anayekuwa Waziri katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Nassor Ahmeid Mazrui (Wizara Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto), pamoja na Omar Said Shaaban atakayeiongoza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Uteuzi wa Mawaziri hao unakamilisha idadi ya Mawaziri 16 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya Wizara hizo tatu kuwa wazi tangu pale Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipotangaza Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza Novemba 19, 2020.
Aidha, Rais Mwinyi amemuapisha Salum Yussuf Ali kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), baada ya kumteua February 10, 2021.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni pamoja na Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na wanafamilia.
Rais Dkt. Mwinyi amewaapisha Viongozi hao kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Vifungu vya 42, 43 (1) (2) na 44 vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.