Baraza la Mawaziri nchini Tanzania, limeagiza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 wakinusurika.
Hayo yamesemwa hii leo Novemba 14, 2022 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa mara baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, na kuongeza kuwa Baraza hilo limetoa maagizo ili kupata chanzo cha ajali na mapendekezo.
Amesema, “Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi wa ajali hii na pia kupata chanzo cha ajali pamoja na mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa mara baada ya ajali kutokea.”
Msigwa amesema Baraza hilo pia limeelekeza vitengo vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe mambo mbalimbali ambayo yatatuwezesha kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya uliopo katika kukabiliana na majanga yanapotokea.
Msigwa, amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na timu ya uchunguzi itakayofanya kazi na kutoa maelezo ndani ya siku 14, ikifuatiwa na ripoti ya awali itakayotolewa ndani ya siku 30 na kisha ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12.
Ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria takribani mita 100 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mkoani Kagera ikiwa na watu 43 waliokuwa wakitoka jijini Dar es Salaam, 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawiliambapo shughuli za uokoaji kwa sehemu kubwa zilifanywa na wavuvi wakiongozwa na kijana Jackson Majaliwa na wenzake waliowezesha watu 24 kuokolewa.