Benchi la ufundi la Young Africans chini ya Kocha Mkuu Mtunisia Nasreddine Nabi na wachezaji wake wote leo Jumamosi saa moja kamili usiku watakuwa kambini wakiwaangalia wapinzani wao watakaokutana nao katika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Young Africans watavaana na Marumo Gallants katika Michuano hiyo ambapo mchezo wa kwanza utachezwa Mei 10, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki moja baadae huko Afrika Kusini.
Mmoja wa mabosi wa Young Africans amesema mara baada ya kikosi kuwasili jijini Dar es salaam jana Ijumaa kikitokea Singida walipokwenda kucheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Singida Big Stars, Kocha Nabi alitoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji wake, na baadae leo Jumamosi watarejea kambini kuanza mawindo ya mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Amesema kuwa lengo la kuwahi kambini ni kuuangalia mchezo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini utakawakutanisha wapinzani wao Marumo Gallants watakaokaribisha dhidi ya Mamelodi Sundowns saa 1:00 usiku.
“Maandalizi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika yalianza mara baada ya mchezo wa mwisho wa Robo Fainali. Kwani malengo yetu yamebadilika hivi sasa ni kucheza fainali na sio nusu fainali tena ambayo hatua tuliyofikia, hivyo hatutaki kupoteza mchezo huu dhidi ya Marumo, hivyo ni lazima tuwajue kwa karibu wapinzani wetu.”
“Hivyo kocha alitoa siku moja ya mapumziko pekee (jana Ijumaa) mara baada ya timu kurejea kutoka Singida na kuwataka wote kesho (leo Jumamosi) hadi kufikia saa kumi wawepo kambini Avic Town kwa ajili ya kuungalia mchezo huo wa Ligi ya Afrika Kusini ambao utakaozikutanisha Mamelodi Sundowns dhidi ya Marumo Gallants,” amesema bosi huyo.
Akizungumzia mchezo huo Nabi alisema: “Tunafahamu mchezo wetu utakuwa mgumu, wachezaji lazima sasa wasahau mafanikio tuliyoyapata kwenye mchezo wa robo fainali na kujiandaa kuwakabili Marumo, hautakuwa mchezo mwepesi, kosa lolote tutakalolifanya linaweza likatuweka kwenye wakati mgumu.
“Nimewaambia wachezaji wangu wanapaswa kusahau mafanikio tuliyoyapata katika mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United, ili kuweza kufanya vizuri kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hii.”
“Naendelea kuwaandaa wachezaji wangu kuweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa nusu fainali na makosa yoyote tutakayoyafanya ndani ya uwanja yatatugharimu,” alisema Nabi.