Kocha wa Juventus FC, Max Allegri anaamini timu hiyo imerejea katika njia sahihi baada ya kupitia misukosuko msimu uliopita.
Allegri aliamua kubaki Juventus akijaribu kutekeleza majukumu ya kuboresha timu kufuatia kashfa iliyotokea msimu uliopita iliyosababisha bodi ya klabu kuvunjika.
Pia klabu hiyo ilikumbwa na adhabu ya kunyang’anywa pointi 10 kufuatia uámuzi mpya wa mahakama ya ltalia unaochunguza kuhusu masuala ya uhamisho wa wachezaji na kukutwa na hatia.
Uamuzi huo ulitangazwa muda mfupi tu kabla ya mechi ya Serie A dhidi ya Empoli kuanza na kuathiri kiwango cha wachezaji waliopoteza mchezo huo kwa mabao 4-1.
Baada ya kupunguziwa pointi ilikatisha matumaini ya wachezaji kumaliza msimu nafasi za juu.
Kabla ya uamuzi mpya, Juventus ilikuwa katika nafasi ya pili chini ya mabingwa wa Serie A, SSC Napoli waliokuwa na pointi 69, lakiní ilishuka hadi nafasi ya saba ikikosa nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Licha ya kupitia changamoto hizo kocha huyo alisema: “Nimerudi na programu sahihi. Katika miaka hii miwili ambayo Juventus haijashinda kombe, nilidhani ingekuwa rahisi zaidi. Kuna makipa watatu tu, na wachezaji saba wa kigeni.
Kwa maoni yangu tumeanza kazi vizuri, lengo ni kuboresha timu. Tulipunguza mishahara ya wachezaji na kufanya usajili pia.”
Allegri alitaja sababu ya kurejea Juventus licha ya timu kupitia kipindi kigumu msimu uliopita akisema: “Napenda kufanya kazi kwa malengo ndio maana nikaridhishwa na kile ambacho kimefanywa katika miaka miwili iliyopita.”