Meneja wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus Max Allegri, amewaondoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kuhusu mshambuliaji Paulo Dybala ambaye hakumaliza mchezo wa jana dhidi ya Sampdoria.
Allegri alifikisha ujumbe huo kwa mashabiki wa kibibi kizee cha Turin, kupita kwa waandishi wa habari aliozungumza nao mara baada ya mchezo huo wa ligi ya Sirie A, ambao ulimalizika kwa Juventus kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.
Alisema mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina hakuptwa na majeraha ya kutisha, hivyo ana matarajio ya kumtumia katika mchezo ujao ya ligi ya Italia dhidi ya SSC Napoli mwishoni mwa juma hili.
“Haimaanishi kila jeraha huwa na ukubwa kiasi ambacho mchezaji atashindwa kucheza mchezo unaofuata, nimezungumza na madaktari wa timu, wamenithibitishia kuwa Dybala atakua Fit kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi.”
“Ni kawaida mchezaji kuumia anapokua katika mapambano ya mechi ama mazoezini, sikushtushwa na tukio la Dybala kutokana na kutambua kazi hiyo ipo chini ya madaktari, ninashukuru atakua sehemu ya wachezaji wangu mwishoni mwa juma lijalo.” Alisema Max Allegri
Bao pekee la Juventus katika mchezo huo lilifungwa na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Colombia Juan Cuadrado katika dakika ya saba.