Klabu ya Crystal Palace imemsajili kiungo kutoka nchini Ujerumani Max Meyer kwa mkataba wa miaka mitatu, kufuatia mkataba wake na klabu ya Schalke 04 kufikia kikomo.

Crystal Palace wamethibitisha kukamilika kwa usajili wa mchezjai huyo aliyekua huru, na wanatarajia ujuzi na maarifa aliyokua nayo akiwa na klabu ya Schalke 04, atauonyesha akiwa na klabu hiyo katika ligi ya England.

Meyer mwenye umri wa miaka 22, anakua mchezaji watatu kujiunga na klabu hiyo ya kusini mwa jijini London katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, akitanguliwa na Vicente Guaita na Cheikhou Kouyate.

“Niliwahi kucheza katika uwanja wa Selhurst Park msimu uliopita nikiwa na klabu Schalke, nilifurahia mazingira ya hapa, niliona yanafaa kwa mchezaji kama mimi, ninaamini ujio wangu katika klabu hii utaleta manufaa makubwa kwa kushirikiana na wachezaji wengine.” Alisema Meyer baada ya kukamilisha usajili wake.

Meyer, amewahi kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani mara nne, na alikuzwa katika kikosi cha vijana cha Schalke kabla ya kupandishwa katika kikosi cha wakubwa ambacho alikifungia mabao 22 katika michezo 192 aliyocheza, ikiwepo michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Aliisaidia klabu hiyo ya nchini Ujerumani kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Bundesliga msimu uliopita.

Katika upande wa timu ya taifa, Meyer alikua miongoni mwa wachezaji waliotwaa medali za fedha wakati wa michuano ya Olimpiki mwaka 2016 na alikuwa miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 na kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2017.

Alianza kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa mwaka 2014, lakini hakubahatika kuitwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka huo, kule nchini Brazil.

Video: Ridhiwani afunguka kuhusu viongozi wa upinzani kuhamia CCM
Ousmane Dembele atua London, akutana na wachezaji wa Arsenal